Friday, July 20, 2012

Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika Ramadhaan

Nasiha Za Minasaba Mbalimbali

www.alhidaaya.com

Nyakati tatu hizi ni muhimu sana za kufanya ibada kutokana na fadhila zake kuu. Mwenye kupenda kuchuma thawabu nyingi asizikose khaswa katika mwezi huu Mtukufu Wa Ramadhaan ambao ni mwezi wenye malipo maradufu

1-Wakati wa mwanzo: Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:

Usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba:

((اللهم بارك لأمتي في بكورها)) الترمذي, أحمد, أبي داود, ابن ماجه

((Ewe Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]

Usimulizi huu umetoka kwa Maswahaba kadhaa ambao wameelezea kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kupeleka kikosi au jeshi aliwapeleka mwanzo wa asubuhi". Vile vile wamesimulia kwamba: "Swakhar alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea biashara zake mwanzo wa asubuhi na matokeo yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata faida kubwa sana".

Wamesimulia Salafus-Swaalih kwamba Ibn 'Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo alipomwambia:

"قُم، أتنام في الساعة التي تقسَّم فيه الأرزاق؟"

"Inuka! Je, unalala katika saa ambayo rizki inagaiwa?"

Ikiwa basi wakati huo ni kama hivyo ilivyoelezwa juu, basi vipi Muislamu auache wakati huu umpite khaswa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhaan?

Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake 'Zaad Al-Ma'aad' amesema: "Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…"

Faida nyingine kubwa ya kubakia macho ukimdhukuru Allaah wakati huu:

Si chini ya muda wa saa na nusu utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah kamilifu:

عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال (( من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة) ) أخرج الترمذي صححه الألباني .

Imetoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jama'ah kisha akakaa anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]

Pindi ukifanya hivyo kwa mwezi mzima utakuwa umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa Ramadhaan? Jitahidi ndugu Muislamu kadiri uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo zingelikukalifu mali, tabu za safari na mashaka ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini kwa Rahma ya Allaah Ametujaalia tuweze kuzichuma tukiwa majumbani mwetu tena kwa wepesi kabisa. Wanaume thawabu zitazidi ikiwa watatekeleza wakiwa misikitini. Wanawake wanazipata fadhila hizo hata wakiswali majumbani mwao. Hata hivyo, pamoja na ujira wote huu, tusisahau kuwa fadhila hizo hazivunji wala hazifuti fardh ya kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa kumetengua wajiibu wake wa kuhiji au kufanya ‘Umrah.

2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi):

Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du'aa yake anayoiomba hairudi:

قال صلى الله عليه وسلم: ((ثلاثة لا ترد دعوتهم: الصائم حتى يفطر والإمام العادل والمظلوم)) وروى الترمذي بسند حسن

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du'aa zao hazirudi; mwenye kufunga hadi afuturu/afutari, Kiongozi muadilifu na aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]

Kwa hiyo ni fursa ya kuitumia Muislamu aombe du'aa na haja zake wakati huu khaswa pia kwa vile ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:

(( وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ)) ((.. na mtakase kwa kumsifu Mola wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa)) [Qaaf: 39]

((وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا وَمِنْ آنَاء اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَى))

((…Na umtakase Mola wako kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha)) [Twaahaa: 130].

(( وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَار))

((…Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako kwa kumhimidi jioni na asubuhi)) [Ghaafir: 55]

3- Wakati wa tatu: Suhuur - Kabla ya Alfajiri

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaaahidi Wacha Mungu Pepo kwa sababu sifa mojawapo yao ni kuomba maghfira kabla ya Alfajiri:

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُون)) ((آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ)) ((كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ)) ((وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُون))

((Hakika wenye taqwa watakuwa katika Mabustani na chemchem)) ((Wanapokea Aliyowapa Mola wao. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema)) ((Walikuwa wakilala kidogo tu usiku)) ((Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira)) [Adh-Dhaariyaat: 15-18]

Kisha wamesifiwa tena kwa sifa hiyo hiyo pamoja na nyinginezo:

((الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالأَسْحَارِ))

((Wanaosubiri, wanaosema kweli, na watiifu, na wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira kabla ya Alfajiri)) [Al-'Imraan: 17]

Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba na kuweko mbingu ya ardhi kutukidhia haja zetu:

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له )) البخاري و مسلم

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Mola wake kumkidhia haja zake na kumuondeshea shida zake? Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache wakati huu ukakupita khaswa kwa vile mwezi huu Mtukufu ambao kila jambo ulifanyalo lina fadhila na thawabu marudufu.

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na nyingine, tuwe katika ibada katika mwezi huu wa Ramadhaan na miezi yote mingineyo na Atujaalie kheri na Baraka nyingi, Atukidhie haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie madhambi yetu yote. Aamiyn.

Thursday, July 12, 2012

Njia 10 Za Kuukaribisha Vizuri Mwezi Mtukufu Wa Ramadhaan

Nasiha Za Minasaba Mbalimbali Anasema Allaah سبحانه وتعالى: ((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ)) (( أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ وَأَن تَصُومُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ)) ((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ)) ((Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama waliyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah))(([Mfunge] siku maalumu za kuhisabika. Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasioweza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua)) ((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala Hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru)) [Al-Baqarah: 183-185] Inatupasa tumshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa Kutujaalia uhai na afya mpaka tunakaribia kufika mwezi mtuku wa Ramadhaan na hii ni fursa nyingine Anayotupa katika maisha yetu kushuhudia mwezi huu na kupata fadhila zake. Na hii ni neema ya Allaah سبحانه وتعالى Ambaye Ametujaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au siku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu zake za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine. Mfano wake ni kama kunapokuwa na mauzo yaliyopunguzwa bei dukani (sale), ambayo kawaida yake huwekwa kwa muda mdogo tu maalum. Na muda huu mtu huweza kununua vitu vingi kwa malipo kidogo tu. Hali kadhalika Ramadhaan, ni mwezi mmoja tu, lakini malipo yake huwa ni mengi kuliko hata malipo ya miezi yote mingine. Ikiwa mtu atatimiza Swawm yake inavyopaswa na kufanya mema mengi, na akawa katika Twa'a (utiifu) kamili na kuomba maghfira, basi hutoka katika mwezi huu akiwa ameghufuriwa madhambi yake. Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم : (( من صام رمضان إيماناً واحتساباً ، غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم ((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim] Ramadhaan ni mwezi ambao tunatimiza Fardhi mojawapo ya Kiislamu. Ni mwezi uliojaa baraka, kheri na Rahma za Allaah سبحانه وتعالى. Kila Muislamu inampasa aukaribishe mwezi huu kwa furaha na matumaini kamili. Zifuatazo ni njia kumi za kujitayarisha kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan na kupata manufaa makubwa pindi utakapotimiza: 1. Du'aa Anza kwa kuomba Du'aa kwamba mwezi huu ukufikie wakati umo katika hali ya siha nzuri na usalama hata uweze kufunga na kufanya ibada zako kwa hamu kubwa na wepesi. 2. Mazoezi katika mwezi wa Sha'abaan Funga Sunnah nyingi katika mwezi wa Sha'abaan, soma Qur-aan Juzuu moja kila siku au chini yake, amka usiku uswali japo Raka'ah mbili, kisha zidisha kidogo kidogo hadi inapoingia Ramadhaan uwe tayari umeshapata mazoezi mazuri. 3. Shukurani Mshukuru Allaah سبحانه وتعالى Kukupa uhai na siha hata uifikie Ramadhaan nyingine. Imaam An-Nawawy alisema, kwamba shukurani inapasa kwa kila jambo jema unalojaaliwa kubwa au dogo na vile vile shukurani inapasa kwa kila jambo baya Analokuepusha nalo Allaah سبحانه وتعالى. Kwa hivyo fanya 'Sajdatush-Shukr' [Sajda ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)] kwa neema hii tukufu. 4. Furaha Furahia kukufikia mwezi wa Ramadhaan kama unavyomfurahikia mgeni mpenzi anapokuja kwako na kumuandalia mazuri yote. Maswahaba رضي الله عنهم, walikuwa wakiamkiana unapoingia mwezi wa Ramadhaan na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisema hivi anapowapa habari nzuri za mwezi wa Ramadhaan: ((جاءكم شهر مبارك افترض عليكم صيامه تفتح فيه أبواب الجنة وتغلق فيه أبواب الجحيم وتغل فيه الشياطين فيه ليلة خير من ألف شهر من حرم خيرها فقد حرم)) رواه أحمد ((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu. Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri] )) [Ahmad] 5. Jipangie wakati na weka maazimio Ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wanafurahia kuingia mwezi wa Ramadhaan kwa kujiandaa kupanga mambo ya kidunia badala ya mambo ya Akhera. Wengi hukimbilia kwenda sokoni kununua nguo za 'Iyd, na kufurahikia vipindi vya Ramadhaan katika televisheni ambavyo sio vya dini kama 'misalsal' (maonyesho ya sinema yanayoendelea [series]), na pia kuanza kukusanya video za filamu, mipira, na mambo ya kupotezea muda usiku wa Ramadhaan. Pia wengine kunua karata, dhumna, meza ya mchezo wa keram kwa maandalizi ya vipumbazo na vipoteza muda katika mchana wa Ramadhaan ili wasiihisi Swawm au kuupeleka muda haraka kama wanavyoamini wao. Badala ya kufanya maandalizi ya kununua misahafu ya ziada, kanda za mawaidha, Qur-aan, kukusanya video za mawaidha na mafunzo mbalimbali ya Dini, vitabu vya Dini kwa lugha wanayoifahamu kwa wepesi na kadhalika. Huu ni mwezi wa kufanya ibada na fursa ya kujichumia mema mengi yamfaayo mtu Akhera. Kwa hiyo ndugu Waislamu, tujitahidi kuutumia wakati wetu wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo: Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda wako wa mchana na usiku. Weka maazimio ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati wote wa mwezi huu. Weka mpango maalum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila kipindi, kusoma Qur-aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja hapa chini. Kama ni mwanafunzi na kama unakuwa ukisoma usiku, lala mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Llayl na usome masomo yako baada ya hapo. Anza mpango wako kwa siku chache na kama unahitaji kurekebisha kuboresha nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua nidhaam ipi itakayowafikiana na hali yako. Nasaha kwa kina Mama na kina Dada: Fanyeni maandalizi mapema ya kununua vyakula vya mwezi wa Ramadhaan na kuviandaa vyenye kuandalika mapema kabla Ramadhaan haijaanza, kama vile; sambusa, madonge ya chapati, maji ya matunda n.k. na kuweka kwenye mashine ya kugandisha barafu (freezer) au jokofu ili ikifika Ramadhaan muwe na kazi chache za jikoni na muweze kupata nafasi kubwa ya kushughulika na Ibaadah mbalimbali kama kusoma Qur-aan, kusikiliza mawaidha na hata kuhudhuria Darsa za Dini. 6. Tawbah na Maghfirah Omba Tawbatun-Nasuuha kwa Mola wako na waombe msamaha wale uliowakosea. Kufanya hivi kutanufaisha zaidi Swawm na Swalah zako na pia kukupa imani kuwa huna haki ya mtu. 7. Jifunze Fiqhi ya Swawm Jifunze elimu ya mambo yanayohusu Swawm (Fiqhi ya funga), hiyo ni muhimu ili usije kufanya jambo la kuharibu Swawm yako. Jifunze Swawm kama aliyokuwa akifunga Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ndio mfano bora kabisa wa kuufuata. Swawm haifunguliwi kwa kula na kunywa tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama kusengenya, kutukana, kugombana. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((من لم يدع قول الزور والعمل به والجهل فليس لله حاجة في أن يدع طعامه وشرابه)) البخاري ((Yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya? Na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji)) [Al-Bukhaariy] 8. Jitayarishe kuchuma mema mengi Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu, huruma, rahma na mapenzi. · Panga kabisa na kuweka kiwango fulani cha kutoa Sadaka na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa ndugu na jamaa. · Kama inakupasa kutoa Zakah, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhaan fanya hima uitimize Fardhi hii pia. · Weka 'azma ya kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu ni thawabu. ((قال صلى الله عليه وسلم : من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألباني ((Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم "Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy na kasahihisha Imaam Al-Albaaniy] · Kama unaye jirani asiye Muislamu, mjulishe kuhusu Ramadhaan, faida na Fadhila zake. Hii ni njia na fursa mojawapo ya kufanya da'awah kwa jirani yako. 9. Hitimisha Qur-aan, Hifadhi na jifunzeTarjama Jipangie wakati uweze kuhitimisha Qur-aan kwani Ramadhaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan na hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Jibriyl عليه السلام kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kusoma naye Qur-aan yote ((عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلم أجود الناس، وكان أجود ما يكون في رمضان حين يلقاه جبريل، وكان يلقاه في كل ليلة من رمضان فيدارسه القرآن؛ ((رواه البخاري ((Kutoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy] Hadiyth hii inatufundisha yafuatayo: Kusoma Qur-aan katika Ramadhaan; Kukutana kwa ajili hiyo; Kupima hifdh yako ya Qur-aan kwa kukaa na Mwalimu au mwenye elimu nzuri ya Qur-aan kwa kukusikiliza au kukufundisha; Kuongeza juhudi za kusoma Qur-aan zaidi katika mwezi wa Ramadhaan: Katika muda wa masaa 24 weka saa moja au mbili khaswa iwe ya Qur-aan kusoma na kujifunza maana ya maneno ya Mola wako uonje ladha ya Qur-aan. Vile vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo sura ndogo ili ukitoka katika Ramadhaan uwe una surah zaidi za kusoma katika Swalah zako. 10. Darsa Hudhuria Darsa katika mwezi huu au soma vitabu vya dini, au sikiliza mawaidha. Jambo hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na bora kabisa katika kuzidisha imani yako. Kwa hakika unahitaji saa tu kuweza kutimiza jambo hili muhimu kila siku. Kama huwezi kuhudhuria msikitini, Alhamdulillah, ALHIDAAYA imewatayarishia mawaidha mengi ya kusikiliza na ya VIDEO. Kwa hiyo badala ya kutazama televisheni na kusikiliza muziki jambo ambalo ni haramu ni bora utazame na kusikiliza mawaidha ujipatie manufaa, thawabu na kuongeza elimu yako. Kumbuka kwamba kama vile mwili unavyohitajia chakula, hali kadhalika Moyo na Nafsi zinahitaji chakula chake nacho ni kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى kwa kila aina ya ukumbusho, na mawaidha na darsa za dini ni mojawapo ya chakula kizuri kabisa cha kutakasa Moyo na Nafsi kwa kuzijaza iymaan na mapenzi ya Mola Wako Mtukufu. Kwa kumalizia, tunasema: Fungua 'Swafha' (Ukurasa) mpya katika maisha yako Baada ya kuweza kuyatimiza hayo yote, bila ya shaka hali yako ya iymaan imekuwa bora kabisa na utakuwa umejibadilisha na kuwa mtu tofauti na ulivyo. Kwa hivyo weka maazimio ya kuendelea hata baada ya Ramadhaan kuwa katika twa'a na ibada, na kuendeleza Qiyaamul-Layl (Swalah za usiku), kusoma Qur-aan japo kidogo KILA SIKU, na iwe umefungua UKURASA MPYA wa maisha yako na kumuomba Allaah سبحانه وتعالى Akuendeleze katika hali hii. Tunachukua Fursa hii ya kuwaombeeni Ramadhaan yenye baraka na kheri nyingi, tutoke katika mwezi huu tukiwa tumesafishwa madhambi yetu yote, na wenye kubeba thawabu nyingi ziwe nzito katika Miyzaan ya Hasanaat (mizani ya amali njema) Siku ya Qiyaamah. اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنّأ وَ مِنْكُم صَالح الأّعْماَل Allaahumma Taqabbal Minnaa wa Minkum Swaalih al-A'amaal. Aamiyn