Thursday, April 10, 2014

Usihuzunike! Baada Ya Dhiki Faraja

Jiepushe Na Moto Wa Jahannam Pamoja Na Familia Yako

Friday, May 10, 2013

Tuishi Kiislam

By ‘Abdun-Naaswir Hikmany Tofauti yetu na wasio kuwa Waislam si chengine kipya ila ni tabia. Uzuri wa mwenendo wa maisha yetu ndio utakaotupatia sifa mbele ya jamii isiyokuwa ya Waislam. Hima yetu ya kutosema uongo na kufuata maadili ya ajabu ndio utakuwa msingi imara wa imani yetu. Haya yote yameelezwa na Habiybul Mustwafaa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hakuletwa yeye isipokuwa kurekebisha jamii kuwa na tabia njema. Hakika Uislamu wetu umekamilika kwa kuwa na tabia bora za kuigwa na Waislam wenyewe kwa ushahidi wa Qur-aan na Sunnah. Kama kweli sisi ni Waislam tunaoipenda diyn yetu ni lazima tuwe tayari kuanza kubadilika kila hatua ya maisha yetu kwa kuishi Kiislam. Zingatio letu litatupeleka hatua baada ya hatua ili kurekebisha nyumba iliyojikita kwenye masuala yasioendana kabisa na mila zetu sisi Waislam. 1. TUZUNGUMZE KIISLAM Muislam wa kweli ni lazima awe ni mkweli, hatakiwi kuzua uongo, kufitinisha, kusengenya wala kuzungumza kwa sauti ya juu. Haya tunayapata ndani ya Qur-aan: {{Na uteremshe sauti yako; bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote (kwa makelele yake ya bure).}} [Surat Luqmaan: 19] Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kushikamana katika kusema ukweli: “Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli unapeleka katika wema, na wema unapeleka Peponi.” [Muslim] 2. TULE KIISLAM Muislam anatakiwa ale kilicho mbele yake kwa kutumia mkono wa kulia na asiwe na papara ya kusukuma tonge namna ya kima anavyokula. Aanze kula kwa kusema “BismiLlaah” na amalize kwa kusema “AlhamduliLlaah”. Chakula cha Muislam ni lazima kiwe ni cha halali, hatakiwi kula ovyo ovyo kama wanavyofanya wasiokuwa Waislam. Anapokula aligawe tumbo lake kwenye thuluthi tatu. Thuluthi moja ni ya chakula, nyengine ni ya maji na mwisho ni hewa. Hii ni kwa mujibu wa dalili ya Hadityh: "Kama ukilazimika kula hakikisha theluthi moja ya tumbo lako unaijaza chakula, theluthi moja maji na acha theluthi moja kwa ajili ya hewa (yaani iache tupu)” (At-Tirmidhiy). 3. TUSIKILIZE KIISLAM Muziki ni haramu na haifai kwa Muislam kuutengeneza, kutengenezewa, kuimba, kuimbiwa, kuutangaza, kuupeleka muziki, kuuza, kula thamani yake, kununua na kuuza. Muziki umekuwa ni tatizo kubwa kwa Waislam kwani wengine hata usingizi hawapati bila ya kusikiliza muziki. Nyumba za Kiislam sasa zimekuwa sawa na magofu kwa kutopatikana maadili ya Kiislam. Kwani wengi wanaishi tofauti na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni muhimu kwa Waislam wakawa wanasoma Qur-aan kila siku kwa sauti na kwa kusikilizana kwa mtindo wa dawaar (mmoja baada ya mwengine). Tuzibadilishe nyumba zetu kwa kusikiliza idhaa za Kiislam zisizokuwa na mambo ya uchafu na uzushi. ((Na soma Qur-aan kwa utaratibu na utungo)) [Al-Muzammil 73: 4] Muislam anayesoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam). Hata yule asiyejua kusoma Qur-aan ni vyema akawa na jitihada ya kujifundisha ilhali anakosea au hata kuchekwa. Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Yule ambaye kwamba anasoma Qur-aan naye ni mjuzi (hana shida aina yoyote) atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam) na watiifu. Na yule ambaye kwamba anarudia pamoja na kuwa na shida katika kusoma basi atakuwa na ujira mara mbili(( [al-Bukhaariy, Muslim, Tirmidhy na Ibn Maajah kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha)] 4. TUVAE NA TUTEMBEE KIISLAM Maringo ya kutembea bila ya shaka yanatokana na mtu kuvaa nguo za kifakhari ambazo hazitakiwi kuvaliwa kwa Muislam. Muislam wa kiume anatakiwa avae nguo zisizoburura. Mwanamke hatakiwi kuonekana zaidi ya viganja vya mikono na kipaji cha sura yake. Mapambo yote ni halali kwa mumewe na walio Maharimu wake. Haitakikani Muislam kutembea kwa kujivuna, kujifakharisha na maringo. Hivi sivyo Uislam unavyotufundisha kuishi. Qur-aan inasema: {{Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala huwezi kufikia urefu wa milima}} [Surat Israa: 37] Usiwaangalie watu kwa jeuri au kwa upande mmoja wa uso. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: {{Wala usiwatazame (usiwafanyie watu jeuri), kwa upande mmoja wa uso, wala usende katika ardhi kwa maringo, hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifaharishaye.}} [Surat Luqmaan: 18] 5. TUJENGE URAFIKI WA KIISLAM Miongoni mwa matatizo makubwa ya vijana wetu pamoja na Waislam kukosa maadili ya Kiislam ni kuwa na marafiki wasiokuwa na maadili mema. Ni vyema Muislam akawa hana rafiki hata mmoja kuliko kuwa na marafiki kumi wasioishi Kiislam. Kuishi Kiislam yatakikana juhudi na inaanza kwa kuwa na rafiki mwema atakayekukemea unapofanya kosa na kukupa maneno ya subra wakati wa huzuni. Lazima tuchague marafiki ambao wako radhi na dini yetu na tuepukane na wale ambao hawako radhi na dini yetu. Na tukiona marafiki zetu matendo yao sio mazuri, ni lazima tuepukane nao kwa sababu tunaweza tukaiga tabia zao ambazo zinakwenda kinyume na dini yetu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mtu yamkini kufuata dini ya rafiki yake, kwa hivyo muangalie unayemfanya rafiki.” (Abuu Daawuud na Tirmidhiy) 6. TULALE KIISLAM Tumalizie kwa kuona namna anavyotakiwa Muislam kuimaliza siku yake kwa kujipumzisha Kiislam. Muislam anatakiwa atie wudhuu kabla ya kulala, wudhuu unaendana na Sunnah ya kupiga mswaki. Ni vizuri ukaswali rakaa tatu za witri (kwa wasioamka usiku). Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akienda kulala usiku anakusanya viganja vyake kisha akivipuliza na akivisomea Suratul-Ikhlaas, na Suratul-Falaq, na Suratu-Nnaas, kisha akipangusa kwa hivyo viganja vyake kiasi anachoweza katika mwili wake, akianza kichwani na usoni na mbele (akifanya hivyo mara tatu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ukienda kulala soma Ayatul-Kursiy mpaka uimalize kwani Mwenyezi Mungu Ataendelea kukuhifadhi wala hakukaribii shetani mpaka asubuhi” Unapolala ulaze ubavu kwa upande wa kulia na usome du’aa ifuatayo: اللّهُـمَّ أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وا جْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت “Ewe Mwenyezi Mungu nimeisalimisha nafsi yangu kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu kwako na nimeutegemeza mgongo wangu kwako, kwa matarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila kwako, nimekiamini kitabu chako ulichokiteremsha na Mtume wako uliyemtuma”. Na hizi hapa ni Nyiradi za kulala. Bila ya shaka tutakapoishi Kiislam tutakuwa mbali na wasiokuwa Waislam. Hivyo maisha yetu yatakuwa hakika ni ya Kiislam. Kila kitu yatakikana juhudi na inaanza kwa nafsi kujifunga kukubali mafundisho ya Kiislam. Inawezekana kubadilika kwa kuishi Kiislam. Anza sasa, katu usichelewe kuishi Kiislam. CREDIT}Alhidaaya

Tuesday, September 25, 2012

KAZI KATIKA UISLAM

Uislamu Na Shari'ah Zake

UTANGULIZI

Kulingana na Kamusi ya Kiingereza ya Collins, kazi imefafanuliwa kama juhudi za kimwili au kiakili zilizoelekezwa kufanya/ kutengeneza kitu, malipo anayopewa kwa amali, biashara, utaalamu, shughuli au ufahamu.

Katika Uislam, kazi inamaanisha juhudi au uajiriwa unaofanywa ili mtu kupata pato la halali na katika mipaka ya maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kanuni Zake. Pale Muislam anapofanya hivyo kwa nia safi na ikhlasi, anapata ujira kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

Katika Uislam dunia ni sehemu ya kuvuna kwa ajili ya Akhera. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

“Na utafute, kwa Aliyokupa Allaah, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Allaah alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Allaah hawapendi mafisadi” (28: 77).

Na Anasema vilevile: “Na Tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha” (78: 11).

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuwekea mchana hasa ili tuweze kuhangaika kimaisha.

Kwa sababu sisi tuko katika ardhi hii, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametufundisha du’aa ifuatayo ya sisi kutaka kheri za nyumba mbili. Anasema Aliyetukuka: “Na katika wao wapo wanaosema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto! Hao ndio watakaopata sehemu yao kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu” (2: 201 – 202).

Waislam katika eneo la Afrika Mashariki wanachukuliwa kuwa sawa na wavivu kwa sababu ya jinsi walivyojiweka katika hali ya uzembe wa hali ya juu. Utawaona vijana wenye miili imara wanakaa mabarabarani, kwenye mabustani na mabarazani, nje ya Msikiti na sehemu nyengine za anasa wakizembea na kuzungumza mambo ya upuuzi. Pia vijana waliohamia nchi za kimagharibi kwa sababu ya ruzuku inayotolewa na serikali wamechukua mienendo hiyo mibaya.

Si halali kwa Muislam kutofanya kazi ili kujikimu kimaisha kwa kisingizio cha kuyaweka maisha yake kuwa wakfu kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah au kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa njia hiyo. Pia haifai kwao kutegemea sadaka japokuwa wana uwezo wa kufanya kazi kwa juhudi na nguvu zao. Katika hili, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sadaka si halali kwa tajiri wala mwenye uwezo wa kimwili” (at-Tirmidhiy).

Katika riwaya nyengine ya Abu Daawuud na an-Nasaa’iy, ‘Ubaydullah ibn ‘Adiyy al-Khiyaar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameripoti: “Watu wawili waliniambia kuwa walikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa Hijjatul Widaa alipokuwa akigawa Zakaah. Walimtaka usaidizi. Aliwatazama kuanzia utosini hadi chini na kuwaona kuwa wamejenga vizuri na wenye nguvu. Aliwaambia: ‘Ikiwa mwataka, nitawapatia (Zakaah), lakini hakuna Zakaah kwa aliye tajiri wala kwa yule mwenye nguvu anayeweza kupata pato”.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza Waislam kuomba omba pasi na dharura yoyote, hivyo kukosa heshima na hadhi. Hili lengo lake ni kuwafundisha na kuwahimiza Waislam kulinda na kuwa mbali na mienendo ya kupe kwa kuwanyonya wenziwe (watu wengine).

HADHI YA KAZI

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anataja misingi inayotakiwa katika kufanya ukulima. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameitandaza ardhi na kuifanya kuwa muruwa na yenye rutuba kwa ajili ya ukulima na kumeza pamoja na kupata mazao. Zipo ayah nyingi kuhusu hilo lakini unaweza kutazama baadhi yake kwa mfano “Na ardhi Tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. Na Tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu” (15: 19-22)

“Na ardhi ameiweka kwa ajili ya viumbe. Humo yamo matunda na mitende yenye mafumba. Na nafaka zenye makapi, na rehani. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayoikanusha” (55: 10-13)

“Na Mwenyezi Mungu Amekukunjulieni ardhi kama busati. Ili mtembee humo katika njia zilizo pana.” (71: 19-20)

“Hebu mtu na atazame chakula chake. Sisi Tumemimina maji kwa nguvu, Tena Tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu, Kisha Tukaotesha humo nafaka, Na zabibu, na mimea ya majani,” (80: 24-28) na kadhalika.

Katika ayah zote hizo kuna kuhimizwa watu kuwa wakulima na kutilia maanani ukulima. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Pindi Muislam anapopanda mti au mmea, hakuna ndege wala mwanaadamu atakayekula kwayo isipokuwa anaandikiwa sadaka” (Al-Bukhaariy na Muslim).

Na katika Hadiyth nyingine anasema: “Kikisimama Qiyaama na mkononi mwa mmoja wenu ana mche akaweza kuumeza basi afanye hivyo kwani atapata ujira kwayo”. Hii ni hima ya hali ya juu aliyotupatia Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata katika wakati mgumu kama huo wa Qiyaama ambapo mambo yote yatabadilika.

Mbali na ukulima, Muislam anaweza kujishughulisha na sayansi za msingi, viwanda na taalamu nyengine kwa idadi kubwa inayoweza kukidhi mahitaji yetu ya kijamii.

Qur-aan imetaja viwanda na taaluma nyingi na kuziita ni fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza kuwa:

Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) alikuwa mfua vyuma hivyo akitengeneza nguo za chuma za kivita.

“Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru”21: 80

“Na tulimpa Daawuuud fadhila kutoka kwetu, (tukasema): Enyi milima! Karirini kumtakasa Mwenyeezi Mungu pamoja naye! Na ndege pia. Na tukamlainishia chuma. (Tukamwambia:) Tengeneza nguo za chuma pana, na kadiria sawa katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika Mimi nayaona vyema mnayo yatenda” (34: 10-11)

Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) alikuwa mjengaji

“Na Sulaymaan tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja. Na tukamyayushia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio kuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anayejitenga na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unaowaka. Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na masanamu, na madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa mahala pake. Enyi watu wa Daawuud! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru” (34: 12-13),

Dhul Qarnayn alitengeneza ukuta mrefu kama kizuizi dhidi ya maadui

“Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora zaidi. Lakini nyinyi nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina yenu na wao. Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie. Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa” (18: 95-97)

Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam) alikuwa seremala

“Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usinisemeze kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli” (11: 37-38).

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) pia Anatutajia merikebu kubwa sana kama milima, ambazo zinavuka baharini

“Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyo kwenda na kurejea baharini kama vilima” (42: 32).

Zaidi ya hayo, Qur-aan imetufahamisha kuwa chuma kina thamani kwa kutilia mkazo jambo hilo.

Anasema Aliyetukuka: “Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu Amjue anaye mnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu” (57: 25).

Kazi yoyote yenye kukidhi mahitaji ya jamii au inayoleta faida ya kihakika inachukuliwa kuwa ni nzuri, ilimradi anayeifanya aifanye kwa njia nzuri, kama inavyotakikana na Uislam. Baadhi ya watu wanazitweza baadhi ya kazi, lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufundisha kuwa heshima na hadhi ya mtu imefungamana na yeye kufanya kazi – kazi aina yoyote ila zile zilizo haramishwa. Hivyo, Uislam ulinyanyua hadhi na vyeo vya kazi nyingi ambazo watu walikuwa wanaziona kuwa duni.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni bora kwa mtu kuchukua kamba na kuleta mzigo wa kuni mgongoni mwake na kuzuiza ili Allaah Ailinde heshima yake, kuliko yeye kuomba kutoka kwa watu bila kujali kama watampatia au watamnyima” (al-Bukhaariy na Muslim).

Ndio yule Swahaba alipokariri kuja kumtaka msaada Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza kama ana akiba yoyote nyumbani kwake. yule bwana akamwambia anacho kitambara. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwagizia akilete, na kilipoletwa alikinadi nacho kikanunuliwa kwa dinari mbili. Moja kati ya hizo dinari mbili Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia anunulie chakula na akiache nyumbani. Ya pili Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe alikwenda sokoni na kununua kile chuma cha shoka na kumtilia mpini kwa mkono wake. Kisha alimwambia asionekane pale mpaka baada ya muda fulani. Swahaba huyo alielekea msituni ili kukata kuni. Baada ya muda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikutana na huyo bwana kukiwa na sauti ya pesa zikilia mfukoni kwake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia hii ni bora kabisa kuliko kuomba omba.

Mitume na Manabii (‘Alayhimus Salaam) ndio ruwaza njema kwetu. Wao walifanikiwa katika kazi zao kwa kiasi kikubwa. Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Daawud alikuwa mtengenezaji makoti ya chuma na ngao zake, Aadam alikuwa mkulima, Nuuh alikuwa seremala, Idriys mshonaji na Muusa mchungaji” (Al-Haakim).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hakumtuma Mtume bila ya yeye kuchunga kondoo”. Wakamuuliza Maswahaba: “Hata wewe, ewe Mtume wa Allaah?” Akajibu: “Hata mimi, nilikuwa nikichunga kondoo wa watu wa Makkah kwa ujira” (Al-Bukhaariy).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia Maswahaba zake hivi ili kuwafunza kuwa heshima inakuwa kwa wale wanaofanya kazi, na sio wale wenye kukaa na kuzembea na kuwa kupe kuwala wengine. Nasi tunaakiwa tufuate mtindo huo wa kufanya kazi. Zipo fursa nyingi, ambazo zinaonekana na sisi Waislam kama ni kazi duni zinazotuteremsha vyeo ambapo wengi wanaishi kwa kufanya kazi hizo na vile vile kuwa na hadhi zao nzuri. Na hivyo kuwa na heshima na hakuna wa kumkebehi au kumdharau kwa kuwa yeye anafanya juhudi na anakula kwa jasho lake.

Uislam umetuhimiza sisi kufanya biashara, na kuziita kutafuta fadhila ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Tafadhali tazama ayah zifuatazo kuhusu mas-ala hayo 2: 198; 24: 37; 28: 57; 73: 20 na kadhalika.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfanya biashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, wakweli na mashahidi” (At-Tirmidhiy na al-Haakim). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe aliweka nidhamu kabambe na kanuni za kibiashara mbali na ghushi (udanganyifu), kuwasilisha kwa namna nyengine, kuficha bidhaa na kufanyiana hiyana.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupigia mfano wa jinsi ndege anavyofanya juhudi kutafuta riziki na akakuita kuwa ni kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika hilo. Hivyo kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni mwanzo kumfunga ngamia kisha kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) asimfanye atoroke. Imepokewa kwa ‘Umar ibn al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Ikiwa nyinyi mtamtegemea Allaah upeo wa kumtegemea basi Atawaruzuku nyinyi kama Anavyomruzuku ndege. Anatoka katika kiota chake asubuhi tumbo lake likiwa tupu na anarudi ikiwa tumbo lake limejaa” (At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Sahihi).

KAZI ZILIZOHARAMISHWA

Uislam umeharamisha baadhi ya kazi, ambazo zinakwenda kinyume na kiini cha misingi yake. Ni haramu kumeza, kula au kuvuta mti kama hashiysh, tumbaku, marijuana, na mihadarati mingineyo ambayo ni haramu kuliwa, kutafunwa au kuvutwa, kwa kuwa mimea kama hiyo haina matumizi mengine ila ya kuleta madhara. Pia si sababu sahihi kwa Muislam kusema anapanda miti au anafuga wanyama kwa ajili ya kuwauzia wasiokuwa Waislam, kwani Muislam haruhusiwi kushiriki katika kueneza vilivyo haramu na vyenye madhara.

Uislam pia umekataza taalamu fulani na viwanda kwa wafuasi wake kwa sababu zina madhara kwa itikadi, maadili, heshima, muruwa na kadhalika. Mfano ni kama ukahaba ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Wala msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zinaa kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Allaah baada ya kulazimishwa kwao huko, Atawasamehe, kwani Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (24: 33).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alikataza hilo, bila kuangalia wala kujali nani atafaidika kwayo. Uislam umekataza dansi, muziki hata nyimbo zenye kuamsha hisia za kiume au kike au shughuli nyingine yoyote kama hiyo, kama nyimbo zenye kuashiria au zilizo chafu au michezo ya kuigiza yenye kuelekeza kwenye uasherati na kadhalika. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).

Utengenezaji wa vileo, mihadarati na masanamu pia umeharamishwa. Uislam umekataza biashara yenye dhulma, udanganyifu, kuongeza faida kubwa sana katika biashara au kueneza vitu vya haramu. Pia ni haramu kufanya biashara ya pombe, nguruwe, masanamu au kitu chengine chochote ambacho utumiaji wake umeharamishwa na Uislam. Wafanya biashara wawe na tahadhari ya kughushi, kugeuza au kuvuruga vipimo na ratili, kuzuilia na kuficha bidhaa ili asiwe ni mwenye kukosa ulinzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Pia atahadhari kwa hilo, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema yafuatayo kuhusu kupunja katika kupima: “Ole wao hao wapunjao! Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe. Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza” (83: 1-3).

Watu wa Madyan, waliotumiwa Mtume Shu‘ayb (‘Alayhis Salaam) ili kuwaonya dhidi ya kupunja wanapopima waliadhibiwa vikali sana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumkadhibisha Nabii wao (Tazama 7: 85-93 na 11: 84-95).

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatoa onyo kali kwa mwenye kuchukua na kutoa riba na Ametangaza vita dhidi yao.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyeezi Mungu, na acheni riba zilizobakia, ikiwa nyinyi ni Waumini, Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyeezi Mungu na Mtume Wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (2: 278-279).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dirhamu moja ya riba ambayo mtu ataitumia kwa kujua ni mbaya zaidi kuliko kufanya zinaa mara 36” (Ahmad).

Haifai kabisa kuficha vyakula ili kupata faida nyingi zaidi au kuficha kasoro ya bidhaa yoyote unayouza.

SIFA NZURI ZA MFANYAKAZI MUISLAM

Mfanyakazi Muislam mzuri ana sifa maridhawa zifuatazo:

1. Mjuzi na Mwenye Elimu: Ujuzi na elimu ni sifa muhimu sana ili shughuli zote ziendeshwe kitaalamu kama inavyotakiwa. Ndio Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam) alimwambia mfalme wa Misri yafuatayo: “Yusuuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi” (12: 55).

2. Uaminifu na Nguvu: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anazungumzia kuhusu tazkiya aliyotoa binti ya mzee mkongwe kwa babake kwa sifa alizokuwa nazo Muusa (‘Alayhis Salaam): “Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu” (28: 26).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfanyabiashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, wakweli na mashahidi” (At-Tirmidhiy na al-Haakim). Muislam ni lazima awe muaminifu katika shughuli zake zote na kutokuwa muaminifu ni kuwa na moja wapo wa alama ya unafiki.

3. Kutunza Vitu vilivyo chini yake: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anamzungumzia Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam) pale aliposema: “Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi” (12: 55).

4. Bidii na Juhudi: Pato la kufanya kwa mikono yako ndio kazi bora kabisa ambayo mtu anaweza kufanya. Imepokewa na Rafi‘ ibn Khadij (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa ni pato gani lililo bora zaidi, naye akajibu: “Ni mtu kufanya kazi kwa mikono yake na kila biashara iliyokubaliwa (na sheria)” (Ahmad na at-Tirmidhiy).

Mitume wote (‘Alayhimus Salaam) walikuwa wakila kwa pato la jasho lao kwa kufanya kazi.

5. Kutunza Wakati wa Kazi: Hii ni sifa ya Muumini aliyejikita katika Iymaan. Mtu anapoanza kazi huwa ana mkataba na mkubwa wa kampuni au shirika na kila mfanyakazi huwa ana masaa yake ya kuwa kazini. Kutotekeleza hilo huwa unajiingiza katika sifa ya unafiki kwani Muislam mwema na mzuri ni yue anayetunza mkataba na ahadi.

SIFA NZURI ZA MWAJIRI MUISLAM

Mwajiri Muislam ni lazima afikirie na azingatie zile hisia za wanaadamu wenziwe. Hivyo, asimtwike mwajiriwa kwa kumpatia kazi au mzigo asiouweza. Tazama jinsi gani yule mzee mkongwe na mcha Mungu alivyomwambia Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam): “Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, khiari yako; lakini mimi sitaki kukutaabisha. InshaAllaah utanikuta miongoni mwa watu wema” (28: 27).

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema yafuatayo kuhusu hayo kama ilivyopokewa na Safwaan kutoka kwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema: “Tahadharini sana, kwani yeyote atakayemdhulumu mtu aliyeandikiana naye mkataba, au akampunja haki yake, au akamlazimisha kufanya kazi ngumu upeo wa nguvu zake, au akamchukulia chochote pasi na idhini yake, mimi nitamtetea Siku ya Qiyaama” (Abu Daawuud).

Mwajiri hafai kumtwika mzigo mkubwa hata mtumwa wake kwa kumpatia kazi zaidi ya uwezo wake, basi mwajiriwa ndio haifai zaidi. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni muhimu sana kumlisha mtumwa, kumvisha (sawa sawa) na kutomtwika mzigo wa kupita uwezo wake” (Muslim).

Katika riwaya ya Imaam Maalik, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amepokea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtumwa anafaa apatiwe chakula na mavazi kwa njia ya kawaida, na anawajibika kufanya zile kazi anazoweza bila ya shida”. Maalik amesema kuwa ‘Umar ibn al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akienda vijijini kila siku ya Jumamosi na pindi anapomuona mtumwa anafanya kazi inayopita uwezo na nguvu zake basi alikuwa akimpunguzia.

Mfanyakazi anatakiwa alipwe ujira au mshahara wake kikamilifu pindi tu anapomaliza kazi yake hiyo au mwisho wa mwezi. Kuhusu hili amepokea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana, lakini mfanyakazi analipwa ujira wake kamili pale tu anapomaliza kazi yake” (Ahmad na at-Tirmidhiy). Na katika riwaya nyengine: “Kabla jasho lake halijakauka”.

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anamchukia na Atakuwa dhidi ya mwajiri asiyelipa ujira au mshahara kwa ukamilifu kwa waajiriwa wake. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Anasema: ‘Nitakuwa dhidi ya watu watatu Siku ya Qiyaama:

1. Mtu anayefanya ahadi kwa jina Langu, lakini anafanya khiyana,

2. Mtu anayemuuza mtu huru (kama mtumwa) na kula thamani yake, na

3. Mwajiri anayemwandika kibarua ambaye anafanya kazi yake kiukamilifu lakini yeye hamlipi ujira wake’” (Al-Bukhaariy).

HITIMISHO

Kwa muono wa Uislam, Waumini wa kweli ni wale wenye kutekeleza amali na kutia bidii katika kazi zao za halali, ambao sifa zao za kipekee ni kuwa shughuli za hii dunia haziwafanyi wao kusahau wajibu wao kwa Mola wao Mlezi. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Allaah, na kushika Swalah, na kutoa Zakaah. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka” (24: 37).

Muislam mzuri ni yule ambaye baada ya amali yoyote ya ‘Ibaadah moja anajitupa uwanjani ili kutafuta fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Na itakapo kwisha Swalah, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Allaah, na mkumbukeni Allaah kwa wingi ili mpate kufanikiwa” (62: 10). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa hima na sisitizo Alilotupatia kwa kazi Hakuiacha hata siku tukufu na siku kuu ya wiki, Ijumaa iwe sisi hatufanyi kazi bali Anataka baada ya Swalah ya Ijumaa tutawanyike katika ardhi ili tufanye kazi na tupate riziki ya halali.

Muislam anapotunukiwa fadhila na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), anafaa amuhimidi na kumshukuru Muumba wake kwa kushikilia amri Zake na kukaa mbali na makatazo Yake. Huu ni mtihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), kwani Yeye Anasema: “Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu” (27: 40).

Lau waajiri Waislam watachukua maagizo haya na kujipamba na sifa tulizozitaja zilizowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na waajiriwa nao wakatekeleza wajibu na majukumu yao basi hakungekuwa na matatizo aina yoyote katika jamii yetu ya Kiislam. Inabidi sisi turudi katika Uislam sahihi uliokamilishwa na Mtume wetu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili tupate kufanikiwa hapa duniani na kesho Akhera.

Friday, August 10, 2012

Laylatul-Qadr- Vipi Uweze Kuupata Usiku Huu?

Tunaingia kumi la mwisho, kumi ambalo ndani yake kuna siku tukufu, siku ya Laylatul-Qadr, ambayo ibada yake ni bora kuliko ibada ya miezi elfu.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

﴿ بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾ (( إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ)) (( وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ)) (( لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ)) ((تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ)) (( سَلَامٌ هِيَ حَتَّى مَطْلَعِ الْفَجْرِ ))

BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym

((Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatul Qadr, (Usiku wa Makadirio[Majaaliwa]). Na nini kitachokujuulisha nini Laylatul Qadr?)) ((Laylatul-Qadr ni bora kuliko miezi elfu)) ((Huteremka Malaika na Roho (Jibriyl) katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo)) ((Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri)) [Al-Qadr: 1-5]

Vile vile dalili katika Hadiyth mbali mbali zimethibiti kuhusu Fadhila za usiku huu mtukufu, na jinsi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa hali yake katika siku hizi kumi za mwisho za Ramadhaan.

Baada ya kuzijua fadhila zake usiku huu mtukufu inakupasa Muislamu ujikaze katika siku kumi hizi za mwisho kuacha mambo yote yanayokushughulisha ya dunia na utumbukie katika ibada tu ili uweze kuupata usiku huo mtukufu, yaani ukukute wewe ukiwa katika ibada ili zihesabiwe ibada zako kama kwamba umefanya ibada ya miezi elfu.

Tukifanya hesabu miezi elfu hiyo ni sawa na umri wa miaka 83!

1000 ÷ 12 = 83.3 yaani miaka themanini na tatu na miezi mitatu takriban.

Hivyo ikiwa Laylatul-Qadr imekukuta katika ibada ya aina yoyote, ikiwa ni Swalah (Qiyaamul-Layl), kusoma Qur-aan, kufanya aina za dhikr, kutoa sadaka, kulisha chakula, kuwasiliana na jamaa, kujielimisha au kuelimisha, kufanya wema kwa watu, yote hayo utaandikiwa kama umefanya hayo kwa umri wa miaka 83! Na juu ya hivyo ibada hiyo ya usiku mmoja tu ni bora zaidi kuliko ibada utakayoweza kufanya miaka 83 na miezi mitatu. Subhaana Allaah!

Jihadhari ndugu Muislamu usije ukakukuta usiku huu mtukufu ukiwa katika maasi au katika sehemu ukiwa umeghafilika na ya dunia kama sokoni, magenge ya soga au michezo ya kupoteza wakati au kwenye televisheni ukiangalia misalsalaat, mipira na sinema zikakupita kheri zote za usiku huu. Utaona siku hizi Waislamu wengi wanashughulika kwenda madukani kutafuta nguo za 'Iyd khaswa kina dada wakiacha masiku haya yawapite wakiwa humo badala ya kuwa majumbani mwao au misikitini kufanya ibada na kutegemea kuupata usiku huu.

Ni siku chache tu ndugu Waislamu ambazo zinakimbia kama upepo. Je, nani basi katika sisi atakayepuuza asiupate usiku huo? Na Nani katika sisi atafanya hima kuupata usiku huo? Kwani hatujui kama tutakuweko duniani mwakani kuzipata siku hizi au hata hatujui kama tutaikamilisha Ramadhaan hii. Basi tujitahidi kwa kukesha siku kumi hizi na kuamsha familia zetu ili iwe kheri yetu kukutana na usiku huo mtukufu tuweze kupata fadhila zake hizo ambazo ni sawa na kulipwa malipo ya umri mrefu kama tulivyoona hapo nyuma hata kama hatutoruzukiwa umri huo.

Mwenye Kuukosa Usiku Huu Amekula Khasara Kubwa

Hakika mwenye kuukosa usiku huo atakuwa amenyimwa kheri zake na itakuwa ni khasara kuukosa usiku huu mtukufu kama anavyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : لَمَّا حَضَرَ رَمَضَان قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ (( قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضَان شَهْرٌ مُبَارَكٌ اِفْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ صِيَامَهُ تُفْتَح فِيهِ أَبْوَاب الْجَنَّة وَتُغْلَق فِيهِ أَبْوَابُ الْجَحِيم وَتُغَلُّ فِيهِ الشَّيَاطِين فِيهِ لَيْلَة خَيْرٌ مِنْ أَلْف شَهْر مَنْ حَرُمَ خَيْرهَا فَقَدْ حُرِمَ)) وَرَوَاهُ النَّسَائِيّ

Kutoka kwa Abu Huraryah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba ilipofika Ramadhaan, amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi elfu. Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa haswa)) [An-Nasaaiy]

Siku hiyo ni siku iliyoteremeshwa Qur-aan kutoka mbingu ya saba hadi mbingu ya kwanza kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala):

﴿ بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾ ((حم)) ((وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ)) (( إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ)) ((فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ))

BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym

((Haa Miym)) ((Naapa kwa Kitabu kinachobainisha)) ((Hakika Tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji)) ((Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima)) [Ad-Dukhaan: 1-4]

Aya ya nne inayosema 'Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikma' kuwa kuna makadirio ya mwaka huo na yote yatakayotokea katika mwaka mzima. Kwa maana kwamba, siku ya Laylatul-Qadr, makadirio yote yaliyomo katika Al-Lawhum-Mahfuudhw (Ubao uliohifadhiwa) na huteremshwa haya makadirio na Malaika ambao wanaandika makadirio ya mwaka unaokuja yakiwa ni kuhusu umri wetu wa kuishi, rizki zetu, na yatakayotokea yote hadi mwisho wake. [Imesimuliwa na Ibn 'Umar, Mujaahid, Abu Maalik, Adh-Dhwahaak na wengineo katika Salaf – Ibn Kathiyr: 8:671]

Kujikaza kufanya ibada

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa inapoingia kumi la mwisho akijikaza kwa kufanya ibada kuliko siku zozote zingine:

عن عائشة – رضي الله عنها- قالت: " كان رسول الله – صلى الله عليه وسلم- يجتهد في العشر الأواخر، ما لا يجتهد في غيره" مسلم

Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijitahidi katika kumi la mwisho kuliko alivyojitahidi katika siku nyingine zozote" [Muslim]

Na katika Swahiyhayn (Al-Bukhaariy na Muslim):

عن عائشة رضي الله عنها، قالت: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلّم إذادخل العشر شذ مئزره، وأحيا ليله، وأيقظ أهله ( وفي رواية) "أحيا الليل،وأيقظ أهله، وجدّ، وشدّ المئزر" رواه البخاري ومسلم،.

Kutoka kwake pia Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha): "Ilipokuwa inaingia kumi (la mwisho) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaza izaar (shuka) yake, akikesha usiku, na akiamsha ahli zake" (Na katika riwaaya nyingine) "Akikesha usiku, akiamsha ahli zake, akijitahidi na akikaza izaar yake" [Al-Bukhaariy na Muslim]

Kwa Nini Umeitwa Laylatul-Qadr?

Amesema Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Llaah):

Kwanza: Kutokana na uwezo nao ni utukufu kama vile kusema “fulani mwenye uwezo mkubwa" yaani mwenye hadhi au utukufu.

Pili: Ni usiku ambao una makadirio ya mwaka mzima na huandikwa yote yatakayotokea mwaka huo, na hii ni Hikma ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na kuonyesha usanifu wa utengenezaji Wake na Uumbaji Wake.

Tatu: Usiku huo una uwezo mkubwa kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

من قام ليلة القدر إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه)) متفق عليه

((Atakayesimama usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Sababu Ya Kupewa Waislamu Laylatul-Qadr

Sababu ya kupewa Ummah huu wetu wa Kiislamu siku hii tukufu ya Laylatul-Qadr ni kwamba:

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliona umri wa Ummah za mwanzo ni mrefu, na umri wa Ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu. [Muwatwtwaa 1/321 (Muhammad Fuad 'Abdul-Baaqy]

Ibada Za Kufanya Masiku Kumi Haya Katika Kukesha

1-Qiyaamul-Layl:(Kisimamo cha usiku kuswali)

((من قام رمضان إيماناً واحتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه)) متفق عليه

((Atakayesimama (Kuswali) Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

2-Kuosma Qur-aan

Khaswa kwa vile usiku wa Laylatul-Qadr ndio usiku ulioteremeshwa Qur-aan kama tulivyoona katika Aayah hizo za juu katika Suratul-Qadr na Suratud-Dukhaan.

Vile vile Ramadhaan nzima inampasa Muislamu asome Qur-aan kwani ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ))

((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi)) [Al-Baqarah: 185]

Na Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alikuwa akimteremkia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila usiku wa Ramadhaan akimsomesha na kumsikiliza Qur-aan:

"كَانَ رَسُولُ اللَّهِ -صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ- أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْآنَ" رواه البخاري

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, na alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy]

3- I'tikaaf

Kutia nia kubakia msikitini kwa kufanya ibada tu humo kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo:

عن عائشة – رضي الله عنها- قالت "كان النبي يعتكف في كل رمضان عشرة أيام؛ فلما كان العام الذي قبض فيه اعتكف عشرين يوماً - أخرجه البخاري

Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba: Mtume (swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya I'tikaaf kila Ramadhaan siku kumi, ulipofika mwaka wake wa kuaga dunia alifanya I'tikaaf siku ishirini" [Al-Bukhaariy]

4-Kuomba Maghfirah

Kwani usipoghufuriwa madhambi yako basi ni hatari!

عَنْ أَنَس وَغَيْره أَنَّ النَّبِيّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَمَّا صَعِدَ الْمِنْبَر ثُمَّ قَالَ (( آمِينَ آمِينَ آمِينَ)) " قِيلَ يَا رَسُول اللَّه عَلَامَ مَا أَمَّنْت ؟ قَالَ (( أَتَانِي جِبْرِيل فَقَالَ يَا مُحَمَّد رَغِمَ أَنْف رَجُل ذُكِرْت عِنْده فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيْك قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل دَخَلَ عَلَيْهِ شَهْر رَمَضَان ثُمَّ خَرَجَ فَلَمْ يُغْفَر لَهُ قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل أَدْرَكَ وَالِدَيْهِ أَوْ أَحَدهمَا فَلَمْ يُدْخِلَاهُ الْجَنَّة قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ )) صحيح الترمذي و قال الشيخ الأباني حسن صحيح

Kutoka kwa Anas na wengineo kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipopanda juu ya minbar aliitikia ((Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn)). Alipoulizwa kwa nini ameitikia hivyo akasema: ((Amenijia Jibriyl akasema: Ewe Muhammad, ole wake yule ambaye unapotajwa hakuswalii, hivyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: ole wake yule ambaye umeingia mwezi wa Ramadhaan kisha akatoka bila ya kughufuriwa, kwa hiyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: ole wake yule ambaye amewakuta wazazi wake au mmoja wa wazazi wake lakini wasimuingize Peponi. Hivyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa Hadiyth hiyo ina daraja ya Hasan Swahiyh]

5-Du'aa Ya Kuomba Maghfirah Katika Siku Kumi Hizi Zakaatul-Fitwr Mwisho

عن عائشة رضي الله عنها أنها قالت يا رسول الله أرأيت إن وافقت ليلة القدر ما أدعو قال: ((تقولين: اَللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌ تُحِبُّ الْعَفْو فَاعْفُ عَنِّي)) ابن ماجه و صححه الألباني Kutoka kwa mama wa waumini bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba alisema "Ewe Mjumbe wa Allaah je, nitakapowafikiswha usiku wa Laylatul-Qadr niombe nini?" Akasema, ((Sema: Ewe Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe)) [Ibn Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy]

Matamshi Yake

Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa Fa'afu 'Anniy

6-Kumkumbuka Allaah Kwa Aina Zozote Za Dhikr

Kwa Tasbiyh, Tahmiyd, Tahliyl, Takbiyr (kusema: Subhaana Allaah, Alhamdulillah, Laa Ilaaha Illa Allaah, Allaahu Akbar)

7- Kuomba Du'aa Na Haja Zako

Kwa vile ni mwezi wa kuomba Du'aa pia kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Ameunganisha Aayah za kufaridhishwa Swawm na Aaya za kuhusu kuomba Du'aa:

((وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ))

((Na waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka)) [al-Baqarah: 186]

Usiku Gani Khaswa Unapatikana Laylatul-Qadr?

Hadiyth zimetaja siku kadhaa ambazo usiku huu mtukufu hutokea katika siku kumi za mwisho na haswa katika usiku wa witiri, zikiwa zimetajwa nyingine kuwa ni usiku wa siku ya ishirini na moja, au ishirni na tatu, au ishirni na tano au ishirini na saba kama ilivyokuja katika dalili zifuatazo:

لحديث عائشة أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((تحروا ليلة القدر في الوتر من العشر الأواخر)) رواه البخاري

Hadiyth kutoka Mama wa Waumini 'Aiashah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku za witiri kwenye siku kumi za mwisho)) [Al-Bukhaariy]

وفي حديث ابن عباس رضي الله عنهما أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: (( التمسوها في العشر الأواخر من رمضان ليلة القدر في تاسعة تبقى ، في سابعة تبقى ، في خامسة تبقى)) رواه البخاري

Hadiyth kutoka Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan, katika (usiku wa) tisa, saba, na wa tano utakaobakia [mwisho wa Ramadhaan])) [al-Bukhaariy]

Imaam Ahmad amerikodi kutoka kwa 'Ubaydah bin As-Swaamit kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu usiku wa Laylatul-Qadr akasema:

((فِي رَمَضَان فَالْتَمِسُوهَا فِي الْعَشْر الْأَوَاخِر فَإِنَّهَا فِي وِتْر إِحْدَى وَعِشْرِينَ أَوْ ثَلَاث وَعِشْرِينَ أَوْ خَمْس وَعِشْرِينَ أَوْ سَبْع وَعِشْرِينَ أَوْ تِسْع وَعِشْرِينَ أَوْ فِي آخِر لَيْلَة ))

((Katika Ramadhaan, utafuteni siku kumi za mwisho, hakika umo katika siku za witiri, siku ya ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano, au ishirini na saba, au ishirini na tisa, au usiku wa mwisho)) [Ahmad]

Alama Zinazobainisha Laylatul-Qadr

1. Kwenye usiku huo kunakuwa na mwanga zaidi. 2. Upepo siku hiyo hutulia, yaani siku hiyo hautokei upepo mkali. 3. Hali ya hewa huwa nzuri. 4. Nyoyo siku hizo huwa na utulivu na unyenyekevu zaidi kuliko siku nyingine. 5. Baadhi ya watu wema huoteshwa usiku kama walivyokuwa wakioteshwa Maswahaba na Salafus-Swaalih (wema waliotangulia)

Asubuhi Yake

حديث أبي بن كعب رضي الله عنه أنه قال : "أخبرنا رسول الله صلى الله عليه وسلم أنها تطلع يومئذ ٍ لا شعاع لها" رواه مسلم

Hadiyth kutoka kwa Ubay bin Ka'ab (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Ametuambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa jua hutoka siku hiyo likiwa halina mishale (mikali)" [Muslim]

(( ليلة القدر ليلة طلقة لا حارة ولا باردة ، تُصبح الشمس يومها حمراء ضعيفة)) صحيح ابن خزيمة

((Laylatul-Qadr usiku ulio katika hali ya ukunjufu, usio na baridi wala joto, asubuhi yake jua huwa jekundu na dhaifu)) [Swahiyh Ibn Khuzaymah]

ليلة القدر ليلة بلجة (أي مضيئة) لا حارة ولا باردة ، لا يرمى فيها بنجم)) (أي لا ترسل فيها الشهب) رواه الطبراني ومسند أحمد

((Laylatul-Qadr usiku wa kung'aa [yaani wenye mwanga] sio joto wala baridi, na vimondo (nyota za kufyatuliwa) hazitotumwa)) [At-Twabaraaniy na Ahmad]

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kukesha masiku haya kumi ili tujaaliwe kuupata usiku huu mtukufu tutoke katika Ramadhaan hii tukiwa tumeghufuriwa madhambi yetu yote na tumepewa fadhila za usiku huu mtukufu zinazolingana na kuongezewa umri wa miaka 83. Aamiyn

Nasiha Za Minasaba Mbalimbali http://www.alhidaaya.com