Jiepushe Na Moto Wa Jahannam Pamoja Na Familia Yako
Anasema Allaah سبحانه وتعالى:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَا يَعْصُونَ اللَّهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ))
((Enyi
mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake
ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi
Allaah kwa Anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa)) [At-Tahriym 6]
'Aliy bin Abi Talhah amepokea kutoka Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba amesema kuhusu Aayah hii: "Mtiini Allaah سبحانه وتعالى na jiepusheni na kumuasi Allaah سبحانه وتعالى na amrisheni familia zenu kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى ili Allaah سبحانه وتعالى Awaokoe na moto wa Jahannam". [At-Twabariy 23: 491]
Kutokana
na Aayah hiyo, ni wajib wa Muislamu kufundisha familia yake; ikiwa ni
mke au mume, watoto, ndugu, wazazi na kadhalika, mambo yaliyo fardhi
kufanya na kuwakataza yaliyoharamishwa.
Hadiyth ifuatayo inathibitisha maana ya Aayah hiyo:
عبد الملك بن الربيع بن سَبْرَة، عن أبيه، عن جده قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((مروا الصبي بالصلاة إذا بلغ سبع سنين، فإذا بلغ عشر سنين فاضربوه عليها(( رواه الإمام أحمد، وأبو داود، وقال الترمذي: هذا حديث حسن.
Imetoka kwa 'Abdul-Malik bin Ar-Rabiy' bin Sabrah kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake kwamba amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Amrisheni watoto kuswali watakapotimia miaka saba, na wapigeni [ikiwa hawatoswali] watakapotimia miaka kumi)) [Imaam Ahmad, Abu Daawuud, na kasema At-Tirmidhy Hadiyth Hasan]
Na
kuwaamrisha watu wako, mfano watoto kuswali ni kudhihirisha mapenzi
yako kwao kwani hutopenda watoto wako waingie motoni, hivyo unapowaonea
huruma asubuhi wasiamke kuswali Swalah ya Alfajiri, sio maana kuwa
unawependa bali ni kinyume chake, kwa vile unawasababisha wawe miongoni
mwa watu wa motoni. Watu wa Peponi watakapowaona watu wa motoni
watawauliza sababu ya kuingia kwao huko motoni na sababu mojawapo
watasema kuwa ni kutokuswali:
((كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ)) ((إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ)) ((فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءلُونَ)) (( عَنِ الْمُجْرِمِينَ)) ((مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَر))َ ((قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ))
((Kila
nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyoyachuma)) ((Isipokuwa watu wa
kuliani) ((Hao watakuwa katika Mabustani, wawe wanaulizana)) ((Khabari
za wakosefu)) ((Ni nini kilichokupelekeni Motoni?)) ((Waseme:
Hatukuwa miongoni waliokuwa wakiswali)) [Al-Mudathhir: 38-43]
Hakika kuamrisha familia zetu kuswali ni jambo gumu sana na ndio maana Allaah سبحانه وتعالى Alipoamrisha jambo hili Alitutaka tuendelee nalo kwani linahitaji kuwa na subira nalo, kama Anavyosema Allaah katika Aayah ifuatayo, ambayo 'Umar ibnul-Khatwaabرضي الله عنه alikuwa akiisoma huku akiamsha familia yake kuswali:
((وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا))
((Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo)) [Twaaha: 132]
Aayah hiyo ya mwanzo inaelezea hali ya huo moto kuwa:
((وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ))
((kuni zake ni watu na mawe))
Watu hao ni sisi wana wa Aadam, na mawe ni masanamu yaliyochongwa yaliyokuwa yakiabudiwa kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:
((إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ))
((Hakika nyinyi na hao mnaowaabudu badala ya Allaah ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu)) [Al-Anbiyaa: 98]
Kisha Malaika wanaowaingiza hao watu motoni hawana huruma kabisa kwa watu waliomkufuru Allaah سبحانه وتعالى, hukimbilia haraka kumtii Allaah سبحانه وتعالى
kuwaingiza watu motoni bila ya kuchelewa hata upepesi wa macho. Malaika
hao wanaitwa Az-Zabaaniya (walinzi wa moto wa Jahannam) kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:
((سَنَدْعُ الزَّبَانِيَة))
((Nasi tutawaita Mazabania!)) [Al-'Alaq: 18]
Basi tujitahidi kutimiza Swalah zetu kama zinavyopasa na kuamrisha familia zetu pia watimize Swalah ili tujiepushe sote na moto huo mkali wa Jahannam.
***********
Source URL: http://alhidaaya.com/sw/node/456
No comments:
Post a Comment