Usihuzunike! Baada Ya Dhiki Faraja
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا)) (( إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ))
((Basi kwa hakika pamoja na ugumu upo wepesi)) ((Hakika pamoja na ugumu upo wepesi)) [Ash-Sharh: 5-6]
Hiyo
ni ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa Mjumbe Wake Muhammad
(Swallah Allaahu 'alayhi wa alihi wa sallam) baada ya kukumbwa na dhiki,
shida na maudhi kutoka kwa watu wake wa Makkah. Akaitimiza ahadi Yake
kwa kumpa faraja ya kupokelewa kwanza na Maanswaari wa Madiynah akaishi
huko kwa amani, kisha Akampa ushindi wa Makkah, na kuuneza Uislam Bara
la Arabuni kote.
Hiyo
vile vile ni ahadi kwetu kutoka kwa Mola wetu kuwa baada ya dhiki na
shida huja faraja. Sio kama ahadi za binaadamu ambazo zinaweza kuvunjwa
zisitimizwe; kanuni zibadilishwe, khiana, hadaa, dhulma na uonevu kufanyika. Lakini ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Haivunjiki na Sunnah Zake hazibadiliki kama Anavyotuhakikishia:
((وَعْدَ اللَّهِ لَا يُخْلِفُ اللَّهُ الْمِيعَادَ))
((Ndiyo ahadi ya Allaah, Allaah Havunji ahadi Yake)) [Az-Zumar: 20]
((فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّهِ تَبْدِيلًا وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّهِ تَحْوِيلًا))
((Basi hutapata mabadiliko katika mwendo (desturi) wa Allaah, wala hutapata mageuko katika mwendo wa Allaah)) [Faatwir: 43]
Allaah (Subhaanahu
wa Ta'ala) Ametoa ahadi kwa kila mwenye kumuomba kuwa Atamuitikia japo
kama itachelewa du'aa yake mtu kukubaliwa. Kuchelewa huko ni kutokana na
Hikma Yake kubwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), kwani yeye Ndiye mwenye
kujua ghayb (mambo ya mbele yasiyoonekana). Hivyo
bila shaka kuna kheri yake kutokutakabaliwa mapema haja zetu, au kuna
shari itakayotukabili pindi haja zetu zikitakabaliwa. Hatuwezi kujua
ingawa kama kawaida ya binaadam huwa na hamu sana na pupa ya kuona haja
zetu zinakubaliwa haraka. Kama Anavyosema:
((وَعَسَى
أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَعَسَى أَن تُحِبُّواْ
شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ وَاللّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لاَ
تَعْلَمُونَ))
((Na
huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu
nacho ni shari kwenu. Na Allah Anajua na nyinyi hamjui)) [Al-Baqarah: 216]
Maafa,
misiba, shida, maradhi, ufakiri, matatizo mbali mbali humkumba
binaadamu na kumuacha akawa katika hali ya dhiki, upweke na huzuni.
Lakini Waislamu tunapaswa tuwe na subira na tawakkul kwa Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) na kuamini maneno Yake kwamba Atatupa faraja tu
baada ya dhiki. Japo kama sio kwa njia ile tuliyomuomba na kuitegemea
lakini hakuna shaka kuwa Atatuokoa katika dhiki hizo kwani Amerudia mara
mbili katika Aayah hizo,
((فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا)) (( إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ))
((Basi kwa hakika pamoja na ugumu upo wepesi)) ((Hakika pamoja na ugumu upo wepesi)) [Ash-Sharh: 5-6]
Faraja
hiyo inaweza kuja kwa njia mbali mbali zaidi ya moja kwani kama
Alivyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu
Aayah hizi kuwa:
((لن يغلب عسر يسرين)) المحدث: ابن حجر العسقلاني إسناده جيد
((Ugumu mmoja haushindi wepesi mbili)) [Ibn Hajar al-'Asqalaaniy ikiwa na isnaad nzuri kama hivyo hivyo kaipa daraja hiyo Shaykh Al-Albaaniy]
Maana
kwamba kwa kila ugumu mmoja kuna wepesi mbili, na ugumu mmoja hauwezi
kushinda wepesi mbili. Kwa maana nyingine ni kwamba, kila shida moja, au
dhiki, au tatizo moja badala yake kuna ufumbuzi zaidi ya mmoja.
Kwa hiyo Usihuzunike ikiwa:
-Umepata msiba wa kuondokewa na kipenzi chako, kwani pengine ni kheri yake kuondoka duniani kuliko kubakia.
-Usihuzunike
mume akikupa talaka bila ya wewe kutaka, au mke akikukataa, kwani
pengine ni kheri yako upate aliye mwenye kheri zaidi ya huyo.
-Ushizunike kwa maradhi yaliyokusibu, kwani kuna walio na magonjwa zaidi ya kwako, na kupewa maradhi ni kutoharishwa na madhambi.
-Usihuzunike
kwa yeyote anayepita kukusengenya, au anayekutukana au kukudhulumu kwa
vyovyote kwani kufanya hivyo anakuchumia thawabu za bure bila ya wewe
kuzifanyia kazi, na kila watu wanapozidi kukusengenya thawabu zao
unapewa wewe, hatimaye yatachukuliwa madhambi yako wajaziwe wao.
-Usihuzunike kwa rafiki uliyemuamimi, ukamfanya kama ndugu yako, lakini kumbe nyuma yako hana moyo msafi na wewe. Au
anayekuhadaa kwa kupita kukutolea aibu zako kwani kufanya hivyo
anajiteremshia hadhi yake kwako na isitoshe anachuma madhambi.
-Usihuzunike ee mzazi, kwa mtoto anayekuasi, endelea kuomba tu kwa Mola wako, kwani du'aa ya mzazi inatakabaliwa.
-Usihuzunike
kwa kuwa ulipoteza umri wako katika maasi, kwani Allaah (Subhaanahu wa
Ta'ala) ni Mwenye kusamehe madhambi ya mja wake. Bali mshukuru kwamba
Amekuruzuku umri hadi sasa ili utubie na uzidishe mema.
-Usihuzunike kuwa katika hali ya umasikini, kwani masikini anayeshukuru ni bora kuliko tajiri mwenye tamaa na dunia.
-Usihuzunike… usihuzunike... usihuzunike, bali kumbuka kuwa kila jambo lina kheri yake:
((لاَ تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ))
((Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu)) [An-Nuur: 11]
Kumbuka na fanya yafuatayo upate kuburudika moyo wako:
1-Omba Du'aa:
Endelea
kumuomba Mola wako, amka usiku uswali Tahajjud nyakati za thuluthi ya
mwisho ya usiku wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anateremka mbingu
ya kwanza kupokea du'aa zetu na kututakabalia. Zamisha moyo wako katika
unyenyekevu, toa joto lako lote, msikitikie, mlilie Mola wako, Yeye
Ndiye mwenye kustahiki kusikitikiwa shida zako na si binaadamu. Endelea
kufanya hivyo kila siku hadi Akufungulie milango ya kheri.
2-Taqwa na Tawakkul:
Ongeza taqwa (Ucha Mungu) na kuwa na tawakkul (mategemezi) kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika kila jambo lako kwani Anasema:
((وَمَن
يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا)) ((وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ
لَا يَحْتَسِبُ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ
اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا))
((Na anayemuogopa (anayemcha) Allaah Humtengezea njia ya kutokea [katika kila tatizo])) ((Na Humruzuku kwa njia (namna) asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah, Yeye Humtosha)) [At-Twalaaq: 2-3]
3-Subira:
Tambua
kuwa kuna thawabu kubwa katika kusubiri mitihani ya Allaah (Subhaanahu
wa Ta'ala). Thawabu hizo Amezitaja sana katika Qur-aan, mojawapo ni:
((إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ))
((Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu)) [Az-Zumar: 10]
4-Amini Qadhwaa (aliyokupangia Allaah) na Qadar (aliyokukadiria) na Ushukuru:
Mshukuru Mola wako kwa mitihani Aliyokujaalia, kwani yote Aliyoyakidhi kwako huwezi kuyarudisha nyuma. Ni bora kukubali Qadhwaa yako na kushukuru kuliko kuendelea kusikitika na kuhuzunika usije ukakufuru.
((مَا
أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي
كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا إِنَّ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ
يَسِيرٌ)) ((لِكَيْ لاَ تَأْسَوْا عَلَى مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا
بِمَا آتَاكُمْ))
((Hautokei
msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika
Kitabu kabla Hatujauumba. Hakika hayo kwa Allah ni mepesi)) ((Ili
msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni)) [Al-Hadiyd:22-23].
5-Aayah na Du'aa za kuondosha dhiki:
Soma sana Qur-aan kwani ni kiburudisho cha moyo cha aina ya pekee:
((يَا
أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء
لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ)) ((قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ))
((Enyi
watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu na poza kuponyesha
yaliyomo vifuani, na uongofu, na Rahma kwa Waumini)) ((Sema: Kwa
fadhila ya Allaah na Rahma Yake! Basi na wafurahi kwa hayo. Haya ni bora
kuliko hayo wanayoyakusanya)) [Yuunus: 57-58]
Bonyeza katika viungo vifuatavyo upate du’aa:
Source URL: http://alhidaaya.com/sw/node/504
No comments:
Post a Comment